Wafon

Wafon (pia hujulikana kama Wadahomey, Fon nu, Agaja; kihistoria waliitwa Jeji na Wayoruba katika jamii ya Waafrika wa uhamishoni huko Amerika Kusini, pia katika maandiko ya kikoloni ya Kifaransa[1][2]) ni kundi la kikabila la lugha za Kigbe.[3][4]
Ni kundi kubwa zaidi la kikabila nchini Benin, hasa kusini mwa nchi hiyo; pia wanapatikana kusini magharibi mwa Nigeria na Togo. Idadi yao inakadiriwa kuwa watu wapatao 3,500,000, na huzungumza lugha ya Kifon, ambayo ni sehemu ya lugha za Kigbe.[3][5]
Historia ya Wafoi inahusiana na ufalme wa Dahomey, ambao ulianza kuwa na mpangilio mzuri kufikia karne ya 17 lakini una mizizi ya kale zaidi inayoshabihiana na ile ya watu wa Aja.[4] Wafon kwa asili walikuwa na utamaduni wa simulizi na mfumo wa kidini wa Kipagani ulioendelezwa vyema.[6] Walijulikana na wafanyabiashara wa Ulaya karne ya 19 kwa utamaduni wa N'Nonmiton, yaani Wanawake wanajeshi wa Dahomey – ambao waliwawezesha wanawake kushiriki jeshini, na baadaye walipigana dhidi ya majeshi ya kikoloni ya Ufaransa mwaka 1890.[7][8]
Miji iliyojengwa na Wafon ni pamoja na Abomey, mji mkuu wa kihistoria wa Dahomey ambao kwa mtazamo wa Wazungu uliwekwa katika Pwani ya Watumwa. Miji hiyo ilikuwa vituo muhimu vya biashara ya watumwa. Sehemu kubwa ya mashamba ya miwa katika Karibi, hasa Haiti, Surinam na Trinidad, ilijazwa na watumwa waliotoka katika Pwani ya Watumwa, kupitia maeneo ya Waewe na Wafon.
Asili
[hariri | hariri chanzo]
Wafon, kama makabila ya jirani Afrika Magharibi, walibakia jamii yenye mashairi ya simulizi hadi mwishoni mwa Karne za kati, bila maandiko ya kihistoria ya kale. Kulingana na simulizi za kihistoria na hadithi zao, Wafon walitokea katika eneo la Tado la leo, mji mdogo wa Wa-Aja uliopo karibu na mpaka wa Togo na Benin. Watawala wao wa mwanzo walikuwa sehemu ya tabaka tawala katika ufalme wa Aja wa Allada (pia uitwao ufalme wa Ardra).[4][9]
Watu wa Aja waligombana vibaya; kundi moja lilijitenga, nao ndio waliokuja kujulikana kama Wa-Fon, waliotembea hadi Allada wakiwa na mfalme Agasu. Wana wa mfalme Agasu walizozana kuhusu nani anapaswa kumrithi baada ya kifo chake, na kundi hilo likagawanyika tena. Safari hii, Wafon walihamia kaskazini hadi Abomey pamoja na mwana wa Agasu, Dogbari, ambapo waliunda Ufalme wa Dahomey karibu na mwaka 1620 BK. Tangu wakati huo, Wa-Fon wameendelea kuishi hapo, huku Ufalme wa Dahomey ukitanuka katika sehemu ya kusini mashariki mwa Benin kwa kuteka falme za jirani.[4]
Simulizi ya kihistoria ya Wafon pia inahusisha chimbuko lao na ndoa za mchanganyiko kati ya kundi hili la Wa-Aja waliotoka Allada-nu kutoka kusini, na wenyeji wa Oyo-nu waliokuwa katika Falme za milimani za Yoruba. Wayoruba walijulikana kama Igede, jina ambalo Wa-Aja waliwapa kama Gedevi.[10][11] Muunganiko wa Wa-Aja waliovamia na wenyeji Wa-Yoruba wa uwanda wa Abomey uliunda utamaduni mpya – wa Wa-Fon.
Ingawa simulizi hizi za asili zimepitishwa kutoka kizazi hadi kizazi, hazikosi utata. Madai ya asili yao kutoka ndani ya Allada hayakuandikwa kwenye vyanzo vya wakati huo kabla ya mwisho wa karne ya 18, na inawezekana yalikuwa jitihada za nasaba tawala ya mji mkuu wa Ufalme wa Dahomey, Agbome, kuhalalisha ushindi wao dhidi ya ufalme wa pwani wa Allada katika miaka ya 1720.[12] Madai hayo pia yanaweza kufasiriwa kama vielelezo vya ushawishi wa kitamaduni na kisiasa kati ya falme badala ya undugu wa kweli.[13]
Historia
[hariri | hariri chanzo]
Ingawa marejeo na historia iliyoandikwa kuhusu Wafon ni haba kabla ya karne ya 17, kuna hati nyingi kuhusu wao kuanzia karne ya 17, hasa zilizoandikwa na wasafiri na wafanyabiashara wa Kizungu waliotembelea pwani za Afrika Magharibi.[14] Kumbukumbu hizo zinataja miji kama Ouidah na Abomey. Miongoni mwa maandiko yaliyoenea sana ni yale ya Archibald Dalzel, mfanyabiashara wa watumwa aliyeandika mwaka 1793 hadithi, historia, na jinsi biashara ya utumwa ilivyofanyika miongoni mwa Wafon, kwenye kitabu chake kiitwacho History of Dahomey (Historia ya Dahomey).[15] Wanazuoni wa kisasa wamehoji kuhusu upendeleo na usahihi wa Dalzel, na kama kitabu chake kuhusu Wafon kilikuwa na lengo la kisiasa au la kielimu tu.[15]
Katika karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20, kadri uwepo wa Wafaransa ulivyoongezeka na kipindi cha ukoloni kilivyoanza katika maeneo ya Benin na jirani, historia na riwaya zilizo na marejeo kwa Wafon zilitokea kwa wingi, kama zile za Édouard Foà,[16] N. Savariau,[17] Le Herisse, na utafiti wa kiajami wa M.J. Herskovits kuhusu Wafon uliochapishwa mwaka 1938.[14]
Historia hizo zinaonesha kuwa Ufalme wa Wafon, yaani Dahomey, ulitanuka mapema karne ya 18, hasa wakati wa utawala wa Mfalme Agaja hadi miaka ya 1740, na kufikia pwani ya Atlantiki kutoka mji mkuu wao wa bara wa Abomey.[4] Katika kipindi hicho, miaka 200 baada ya Wareno kuweka makazi katika ardhi ya Wakongo katika pwani ya Atlantiki ya Afrika ya Kati katika karne ya 16, tayari kulikuwa na mashamba mengi ya biashara katika Karibi na pwani ya Atlantiki ya Amerika ya Kusini, yenye mahitaji makubwa ya watumwa kutoka kwa wafanyabiashara wa Kizungu. Eneo jipya la Dahomey lilikuwa na nafasi nzuri ya kusambaza watumwa kwa biashara hiyo ya kuvuka Atlantiki, na historia ya karne ya 18 na 19 ya watu wa Fon inaelezewa kwa muktadha huu.[4][18][19]
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Albéca, Alexandre L. d' (1889). Côte occidentale d'Afrique: les établissements français du golfe de Bénin : géographie, commerce, langues : carte au 1/200,000 (kwa Kifaransa). L. Baudoin.
- ↑ Lima, Vivaldo da Costa (2003). A família de santo nos candomblés jejes-nagôs da Bahia: um estudo de relações intragrupais (kwa Kireno (Brazili)). Corrupio. uk. 46. ISBN 978-85-86551-17-8. Iliwekwa mnamo 4 Machi 2025.
{{cite book}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ 3.0 3.1 Fon people, Encyclopædia Britannica, haijatajwa tarehe, idadi ya watu milioni 1.7, Imetazamwa Juni 29, 2019
- ↑ 4.0 4.1 4.2 4.3 4.4 4.5 Elizabeth Heath (2010). Anthony Appiah; Henry Louis Gates (whr.). Encyclopedia of Africa. Oxford University Press. ku. 482–483. ISBN 978-0-19-533770-9.
- ↑ III, John A. Shoup (2011). Ethnic Groups of Africa and the Middle East: An Encyclopedia: An Encyclopedia (kwa Kiingereza). ABC-CLIO. ISBN 978-1-59884-363-7.
- ↑ Molefi Kete Asante; Ama Mazama (2009). Encyclopedia of African Religion. Sage Publications. ku. 270–273, 257, 412. ISBN 978-1-4129-3636-1.
- ↑ Robin Law (1993), The 'Amazons' of Dahomey, Paideuma: Mitteilungen zur Kulturkunde, Bd. 39 (1993), uk. 245–260
- ↑ Alpern, Stanley B. (1998). "On the Origins of the Amazons of Dahomey". History in Africa. 25. Cambridge University Press: 9–25. doi:10.2307/3172178. JSTOR 3172178. S2CID 162412301.
- ↑ Patrick Taylor; Frederick I. Case (2013). The Encyclopedia of Caribbean Religions. University of Illinois Press. ku. 742–746, 1134–1139. ISBN 978-0-252-09433-0.
- ↑ "The Kingdom of Abomey, the Royal Palaces of Abomey - Evenemenciel". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2017-09-02. Iliwekwa mnamo 2017-09-02.
- ↑ Sandra T. Barnes (1997). Africa's Ogun, Second, Expanded Edition: Old World and New. Indiana University Press. uk. 49. ISBN 0-253-11381-4.
- ↑ Law, Robin (1991). The Slave Coast of West-Africa 1550-1750. Oxford: Clarendon Press. uk. 27. ISBN 0-19-820228-8.
- ↑ Miller, Joseph C. (1980). The African Past Speaks: Essays on Oral Tradition and History. Folkestone: Archon Books. uk. 31-4. ISBN 0208017844.
- ↑ 14.0 14.1 Patrick Manning (2004). Slavery, Colonialism and Economic Growth in Dahomey, 1640-1960. Cambridge University Press. ku. xv–xvi. ISBN 978-0-521-52307-3.
- ↑ 15.0 15.1 I. A. Akinjogbin (1966), Archibald Dalzel: Slave Trader and Historian of Dahomey, The Journal of African History, Cambridge University Press, Vol. 7, No. 1 (1966), kurasa 67-78
- ↑ Le Dahomey, Édouard Foà (1895), BnF: Maktaba ya Kitaifa ya Ufaransa (kwa Kifaransa)
- ↑ L'agriculture au Dahomey N. Savariau (1906), A. Challamel, Marseille, Ufaransa, Maonyesho ya Kitaifa (kwa Kifaransa)
- ↑ Law, Robin; Mann, Kristin (1999). "West Africa in the Atlantic Community: The Case of the Slave Coast". The William and Mary Quarterly. 56 (2): 307. doi:10.2307/2674121. JSTOR 2674121.
- ↑ Herbert S. Klein (26 Aprili 2010). The Atlantic Slave Trade. Cambridge University Press. ku. 53, 64–65, 53–68. ISBN 978-1-139-48911-9.
{{cite book}}
: CS1 maint: date auto-translated (link)