Britania

Britania (pia Britania Kuu ni kisiwa katika Bahari ya Atlantiki ya Kaskazini, kilicho nje ya pwani ya kaskazini-magharibi ya bara la Ulaya. Kina nchi za Uingereza, Uskoti, na Welisi. Kwa eneo la kilomita za mraba 209,331 (maili za mraba 80,823), ndicho kisiwa kikubwa zaidi katika Funguvisiwa la Britania, kisiwa kikubwa zaidi cha Ulaya, na kisiwa cha tisa kwa ukubwa duniani. Kina hali ya hewa ya baharini yenye tofauti ndogo za joto kati ya misimu.
Britania iko kati ya Bahari ya Eire (Ireland) na Bahari ya Kaskazini. Pamoja na visiwa vya Eire (Ireland), ambacho kiko upande wa magharibi kikiwa na asilimia 40 ya ukubwa wa Britania Kuu, Faroe, kisiwa cha Man na visiwa vidogo zaidi ya 1,000 vilivyoizunguka na miamba mikubwa iliyopewa majina, ni sehemu ya funguvisiwa la Britania.
Britania hutenganishwa na Ulaya bara kwa Mfereji wa Kiingereza. Mji wa Dover katika Uingereza ya kusini una umbali wa km 34 na mji wa Calais katika Ufaransa.
Jina la Britania limetokana na Waroma wa Kale waliovamia kisiwa na kufanya sehemu ya kusini kuwa jimbo la dola lao. Jimbo la Britania ya Kiroma lilienea katika nchi za Uingereza na Welisi za leo.
Kisiwa chote ni sehemu ya Ufalme wa Muungano unaoitwa mara nyingi "Uingereza" kutokana na nchi kubwa ndani yake. Lakini ufalme huo ni mkubwa kushinda Britania, uko pamoja na Eire ya Kaskazini, visiwa vya Hebridi, Orkney na Shetland, halafu maeneo ya ng'ambo. Hizi zote si sehemu ya Britania lakini ziko pamoja katika Ufalme wa Muungano.
Visiwa katika mfereji wa Kiingereza (Jersey na Guernsey) na kisiwa cha Man viko chini ya mfalme wa Uingereza lakini si sehemu za Ufalme wa Muungano.
Britania huitwa pia "Britania Kuu" kwa sababu ya "Britania ndogo" katika Ufaransa (Kiingereza: "Brittany"; Kifaransa: "Bretagne").
Mara nyingi neno "Uingereza" linatumiwa kutaja kisiwa chote kwa sababu Uingereza ni nchi kubwa kisiwani.
Tanbihi:
- Redio Tanzania imependekeza neno moja la "Uingereza“ kwa ajili ya nchi, kisiwa na pia dola
- TUKI imependekeza maneno mawili ya Uingereza (kwa nchi pia kwa ajili ya Ufalme wa Muungano) na Briteni (kwa ajili ya kisiwa); lakini "Briteni“ ina matatizo kwa maandishi ya kihistoria na kijiografia kwa sababu inafanana mno na jina la "Brittany“ au "Bretagne“.
- Makala hii inajaribu kutumia neno la "Britania“ na kusubiri michango ya wanawikipedia.
![]() |
Makala hii kuhusu maeneo ya Ulaya bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Britania kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |