Nenda kwa yaliyomo

Manikongo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mchoro wa Manikongo.

Manikongo (pia: Mwene Kongo au "Mwenye Kongo" yaani "Bwana wa Kongo") ilikuwa cheo cha mtawala wa Ufalme wa Kongo kati ya Karne ya 14 na ile ya 18 katika maeneo ambayo leo ni sehemu za Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mji mkuu wa Manikongo ulikuwa M'banza-Kongo (uliitwa Sao Salvador miaka 1570-1975) ambao leo ni makao makuu ya jimbo la Zaire la Angola.

Hakuna uhakika umbo la neno lilitokea namna gani; labda lilikuwa tu njia ya Wareno ya kuandika "Mwene Kongo". Lakini umbo hilo lilitumika katika maandiko na nyaraka zilizotumwa kati ya Manikongo na Wafalme wa Ureno zilizohifadhiwa hadi leo.

Mwene Kongo alichaguliwa na akina "bambuta" au wazee wa ufalme. Vyeo mbalimbali chini yake viligawiwa kufuatana na mapokeo kati ya wawakilishi wa koo muhimu.

Manikongo wa kwanza alikuwa Lukena lua Nimi (1380 - 1420) aliyeanzisha ufalme.

Nzinga Nkuwu (1482-1505) alikuwa mwene Kongo wa sita aliyeanza kuwasiliana na Ureno. Akawa Mkristo mwaka 1491 na kutumia jina la Kireno João I (Yohane I).

Mfalme wa mwisho wa Kongo huru alikuwa Pedro V (1859-1891) aliyepaswa kukubali ubwana wa mfalme wa Ureno.

Uwezo wa Manikongo ulipungua kadiri uwindaji wa watumwa ulivyoharibu utaratibu wa ndani na kuwapa wakubwa moyo kupinga mamlaka ya mfalme. Watumwa wengi walichukuliwa na kupelekwa kwenye mashamba ya miwa nchini Brazili. Kazi hiyo ilifanywa vikubwa na wakoloni Wazungu na kusababisha kupungua kwa watu katika ufalme huu.

Baada ya mwisho wa ufalme cheo kimeendelea kwa maana ya kiutamaduni hata wakati wa ukoloni na uhuru.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]