Ngeda
Ngeda | ||||||||||||||||||||
---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|
![]() Ngeda wakipandana
| ||||||||||||||||||||
Uainishaji wa kisayansi | ||||||||||||||||||||
|
Ngeda (Zonocerus elegans) ni spishi ya panzi ya familia Pyrgomorphidae. Spishi za familia hii inaitwa panzi wa kuvutia pia. Kuna spishi nyingine, Zonocerus variegatus, inayotokea Afrika ya Magharibi mpaka Uganda. Spishi hii inaonekana hasa kwenye kanda ya misitu, lakini ngeda huishi maeneno makavu zaidi. Inasambaa Afrika ya Mashariki na ya Kusini na Madagaska.
Maelezo
[hariri | hariri chanzo]Wapevu wa ngeda wana urefu wa sm 4-5 (majike) na 3-4.5 (madume). Wana rangi nyingi: njano, kijani, buluu, nyeusi, nyeupe, machungwa na nyekundu. Rangi hizi huitwa aposemetiki inayomaanisha kwamba zina onyo la ladha mbaya sana hata ya kisumu. Mabawa ya mbele ni kijani na yale ya nyuma ni mekundu msingini kwao au mekundu mazima yakiwa mafupi sana. Rangi hii huonekana kupitia mabawa ya mbele. Macho ni mekundu na vipapasio vina miviringo myeusi na machungwa kwa mbadala. Uso na miguu ni myeusi yenye madoa njano na meupe. Fumbatio ina miviringo myeusi na njano.
Mabawa ni mafupi kwa kawaida, kwa hivyo hawawezi kuruka nayo. Hata kuruka na miguu yao ya nyuma hawawezi vizuri sana. Asilimia ndogo ya panzi hawa ina mabawa marefu lakini mafupi kuliko fumbatio. Hata hawa hawaruki juu vizuri. Hawana haja sana ya kukimbia kwa sababu ya ladha yao mbaya. Mbuai akiionja mara moja hatagusa ngeda tena.
Tunutu wa ngeda ni weusi wenye madoa meupe na njano. Wana ladha mbaya vilevile kama wapevu. Kuna hatua tano za tunutu, kisha hubadilika kuwa wapevu.
Mzunguko wa maisha
[hariri | hariri chanzo]Wapevu wa ngeda huonekana mwanzoni mwa mwaka wakati wa msimu wa mvua. Madume hupanda majike na hukaa pamoja hadi mayai yametagwa ardhini. Hawa hudumu huko kwa muda wa miezi 7-9. Mvua ikirudi mwezi wa Oktoba, tunutu huibuka kutoka mayai. Katika kipindi cha miezi 2.5-3.5 wanapitia hatua tano kabla ya kubadilika kuwa wapevu. Nyakati ni tofauti kidogo katika Afrika ya Kusini kwa sababu ya tofauti ya tabianchi.
Ekolojia
[hariri | hariri chanzo]Ngeda ni panzi wa savana na hatokei misitu mizito wala maeneo makavu sana. Chakula chao muhimu ni mimea yenye sumu, kama mtikiti-jangwa (Citrullus colocynthis) na spishi za Asclepias (milkweed). Sumu za mimea hiyo huingizwa ndani ya mwili wa ngeda ili kupata ladha mbaya. Hata hivyo, ngeda hula spishi nyingi za mimea. Wanaweza kuwa wasumbufu shambani mwa wakulima, lakini hasara ni kwa mahali tu, kwa sababu hawawezi kuenda mbali kwa mwendo wao wa polepole na bila mabawa na kwa hivyo hawasambai mbali. Mazao wanayoweza kushambulia ni muhogo hasa na pia mgomba, mpamba, mnjugu, mnanasi, miti ya matunda n.k.
Tunutu, hasa wale wadogo, huwa na kukusanyika kwenye vilele vya mimea. Labda hii inatisha mbuai wadogo, na wakubwa hugundua upesi kwamba tunutu hawa wana ladha mbaya. Kwa wakulima inawarahisishia kuwapata na kuwashughulikia. Tunutu wakubwa huanza kuenea na kwa hiyo wapevu hawataunganishwa sana, ingawa msongamano wao unabaki juu kiasi, kwa sababu hawasogei haraka.
Udhibiti
[hariri | hariri chanzo]Mara nyingi hakuna haja ya kudhibiti ngeda, kwa sababu hasara zako ni ndogo kwa kawaida. Hata hivyo, ni wazo zuri kuondoa makundi yote ya tunutu mtu anayogundua. Si lazima kutumia dawa za kikemia. Dawa za kienyeji zinatosha au hata kuwachoma. Ikiwa uvamizi umekuwa mbaya, dawa zenye kiwango cha chini cha sumu zinaweza kutumika. Kuna dawa ya kibiolojia iliyo na kuvu kidusia ndani yake, inayoitwa Metarhizium acridum. Inauzwa nchi kadhaa za Afrika kwa jina la Novacrid, lakini kwa sasa (2025) haijasajiliwa Afrika ya Mashariki.
Picha
[hariri | hariri chanzo]-
Jike lenye mabawa mafupi
-
Dume lenye mabawa mafupi
-
Jike lenye mabawa marefu
-
Tunutu wa hatua nne