Nenda kwa yaliyomo

Uajemi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Iran)
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
جمهوری اسلامی ایران Jomhuri-ye Eslâmi-ye Irân (Kifarsi)
Kaulimbiu: اَللّٰهُ أَكْبَرُ Allāhu Akbar (kisheria)
Uhuru, Haki, Jamhuri ya Kiislamu (kiutendaji)
Wimbo wa taifa: Sorud-e Melli-ye Jomhuri-ye Eslâmi-ye Irân
Mahali pa Uajemi
Mji mkuu
na mkubwa
Tehran
Lugha rasmiKifarsi
 • Kiongozi Mkuu
Ali Khamenei
 • Rais
Masoud Pezeshkian
Historia
 • Mapinduzi ya Kiislamu
11 Februari 1979
 • Katiba ya sasa
3 Desemba 1979
 • Marekebisho ya katiba
28 Julai 1989
Eneo
 • Jumlakm2 1,648,195 (ya 17)
 • Maji (asilimia)1.63%
Idadi ya watu
 • Kadirio la 202485,961,000
 • Msongamano52/km2
PLT (PPP)Kadirio la 2024
 • Jumla $1.698 trilioni
 • Kwa kila mtu $19,607
PLT (Kawaida)Kadirio la 2024
 • Jumla $434.243 bilioni (ya 37)
 • Kwa kila mtu $5,013
HDI (2023) 0.799 .
- juu
Gini (2022)34.8
SarafuRial ya Iran (IRR)
Majira ya saaUTC+3:30 (IRST)
Upande wa magariKushoto
Msimbo wa simu++98
Jina la kikoa.ir

Uajemi (pia Iran; jina rasmi: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa Kifarsi: جمهوری اسلامی ایران) ni nchi iliyoko katika Asia ya Magharibi. Inapakana na Armenia, Azerbaijan, na Bahari ya Kaspi upande wa kaskazini; Afghanistan na Pakistan mashariki; Iraq na Uturuki magharibi; Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman kusini. Iran ina eneo la takriban kilomita za mraba 1,648,195, na ni nchi ya pili kwa ukubwa katika Mashariki ya Kati. Inakadiriwa kuwa na idadi ya watu zaidi ya milioni 88, na mji wake mkuu na mkubwa zaidi ni Tehran. Uajemi ina historia ndefu ya ustaarabu wa kale kama milki ya Achaemenid, Sasani, na pia imekuwa kitovu muhimu cha utamaduni, fasihi, na falsafa katika ulimwengu wa Kiislamu na kimataifa.

Iran imekuwa na historia ya kisiasa iliyojaa mageuzi na migogoro, hasa katika karne ya 20. Baada ya mapinduzi ya Kikatiba ya 1906, Iran ilianzisha mfumo wa Ufalme wa kikatiba, lakini ushawishi wa kigeni kutoka kwa Uingereza na Urusi uliendelea kuathiri sera za ndani. Mnamo mwaka 1979, Mapinduzi ya Kiislamu yalitokea na kuiondoa utawala wa kifalme wa Mfalme Mohammad Reza Pahlavi, na kuasisi Jamhuri ya Kiislamu chini ya uongozi wa Ayatollah Ruhollah Khomeini. Tangu wakati huo, Iran imekuwa chini ya mfumo wa kipekee wa uongozi wa kidini na kisiasa, ambapo Kiongozi Mkuu ndiye mwenye mamlaka ya juu zaidi kuliko rais.

Katika karne ya sasa, Iran imekuwa ikikumbwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii, hasa kutokana na vikwazo vya kimataifa vinavyohusiana na mpango wake wa nyuklia. Pamoja na hayo, nchi hii imeendelea kuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa na kiutamaduni katika Mashariki ya Kati, hasa kupitia uhusiano wake na makundi na mataifa ya Kiislamu. Iran pia ni mzalishaji mkubwa wa mafuta na gesi asilia, na rasilimali hizo zimekuwa nguzo kuu ya uchumi wake. Licha ya mivutano ya kimataifa, taifa hili linaendelea kuwa mhimili muhimu katika siasa za kanda na katika Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote.

Historia

Tangu mwaka 500 KK makabila madogo ya nchi yaliunganishwa, na hii ilikuwa mwanzo wa milki ya Uajemi. Mfalme Koreshi II aliunganisha Uajemi wote chini ya mamlaka yake akavamia sehemu za Uturuki wa leo na Babeli na kuunganisha nchi hizo.

Waandamizi wake walipanua milki hadi Misri, Uhindi na Ugiriki.

Milki hiyo ilikwisha baada ya kushindwa na Aleksanda Mkuu; lakini nasaba za Waparthia na Wasasanidi walifufua milki ya Uajemi tena na tena.

Baada ya uvamizi wa Waarabu Ujaemi wkatawaliwa kwa muda kama sehemu ya ukhalifa wa Uislamu lakini baada ya karne kadhaa nasaba za kieneo zilichukua utawala kwa jina la khalifa ila hali halisi kama watawala wa kujitegemea.

Baada ya uvamizi wa Wamongolia nasaba ya wana wa Timur iliunganisha Uajemi pamoja na Afghanistan na Asia ya Kati.

Tangu mwaka 1600 kitovu cha utawala kilirudi Uajemi wenyewe chini ya nasaba za Safawi na Khadjari.

Baada ya vita kuu ya kwanza ya dunia afisa wa kijeshi Reza Khan alimaliza utawala wa Wakhadjari akaanzisha nasaba ya Pahlavi. Alijaribu kuleta matengenezo ya kimaendeleo nchini akaiga katika mengi mfano wa Atatürk katika Uturuki jirani.

Utawala wa kifalme ulikwisha mwaka 1979 wakati wa mapinduzi ya Kiislamu chini ya uongozi wa Ayatollah Khomeini yaliyoanzisha Jamhuri ya Kiislamu.

Kipindi kifupi baada ya mapinduzi Uajemi ilishambuliwa na Iraki na vita vya miaka 8 ilisababisha vifo vingi.

Uhusiano na nchi za magharibi, na hasa Marekani, umekuwa mgumu tangu mapinduzi, hasa baada ya wanafunzi Waajemi kushambulia ubalozi wa Marekani mjini Teheran na kuwateka Wamarekani kama makole. Fatwa ya Ayatollah Khomeini kudai kifo cha mwandishi Salman Rushdie iliongeza sifa za ukali za Uajemi.

Tangu uchaguzi wa Rais Mahmoud Ahmadinejad mwaka 2006 aliyetamka matishio dhidi ya nchi ya Israeli kuna mashaka juu ya mipango ya Uajemi kupanua teknolojia yake ya kinyuklia kwa hofu ya kwamba serikali yake inalenga kujenga bomu ya nyuklia. Mapatano yalichukua miaka hadi kufikiwa mwaka 2015.

Utawala

Uajemi ni Jamhuri ya Kiislamu inayoongozwa na katiba yenye sehemu za kidemokrasia na sehemu za kidini.

Mamlaka kuu iko mikononi mwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi anayesimamia siasa ya nchi kwa jumla; yeye ni amiri jeshi mkuu na msimamizi mkuu wa huduma ya usalama; pia anaratibu siasa ya nje. Anateua wakuu wa jeshi, redio na televisheni, viongozi wa salat wa msikiti mkuu katika kila mji, jaji mkuu na mwendesha mashataka mkuu halafu nusu ya wajumbe wa Halmashauri ya Walinzi wa Katiba wanaokubali au kukataa sharia zote zilizopitishwa bungeni wakiwa na mamlaka kusimamisha wagombea kwa uchaguzi wa kitaifa. Anaweza kumwachisha rais. Kiongozi mkuu huchaguliwa na Mkutano wa Wataalamu wa Uongozi kwa muda wa maisha yake. Ayatollah Khamenei ni Kiongozi Mkuu wa pili tangu mapinduzi ya Kiislamu.

Serikali inayoongozwa na rais wa Uajemi aliye na nafasi ya pili baada ya Kiongozi Mkuu. Huchaguliwa na wananchi wote kwa kipindi cha miaka 4 na anaweza kuchaguliwa upya. Wagombea wanahitaji kukubaliwa na Halmashauri ya Walinzi wa Katiba. Rais anaongoza serikali na kazi yake. Katika mambo ya siasa ya nje, jeshi na siasa ya nyuklia yuko chini ya mamlaka ya kiongozi mkuu.

Bunge inayoitwa "majlis" ina wabunge 290 waliochaguliwa kwa muda wa miaka 4. Wagombea wote wanahitaji kibali cha Halmashauri ya Walinzi wa Katiba. Majlis inatunga sheria za nchi na kukubali makisio ya serikali na mikataba ya kimataifa. Sheria zote zilizopita bungeni zinahitaji tena kibali cha halmashauri ya walinzi.

Halmashauri ya Walinzi wa Katiba ni chombo muhimu sana kinachohakikisha mamlaka kuu ya kiongozi mkuu. Ina wajumbe 12 ambao ni wanasheria. 6 wanateuliwa moja kwa moja na Kiongozi Mkuu. 6 wengine wanachaguliwa na bunge kati ya majina wanaopelekwa mbele na jaji mkuu - anayeteuliwa na Kiongozi Mkuu. Kwa hiyo kiongozi mkuu anaamua juu ya wajumbe wote waliomo katika halmashauri hii, hakuna anayeweza kuwa mjumbe bila kibali chake ama moja kwa moja au kupitia jaji mkuu aliyeteuliwa naye.

Mikoa

Uajemi umegawiwa kwa mikoa 31 inayoitwa "ostan" chini ya gavana anayeteuliwa na rais. Kila mkoa huwa na wilaya (shahrestan) na ngazi ya chini zaidi ni mitaa (bakhsh). Chini ya mitaa kuna kata (dehestan) zinazojumlisha vijiji kadhaa.

Watu

Iran ina mchanganyiko wa makabila na dini uliounganishwa na utamaduni na lugha ya Kiajemi, ambayo inatumiwa na wananchi walio wengi na ndiyo lugha rasmi, ikifuatwa na lugha nyingine za jamii ya Kihindi-Kiulaya, lakini pia za jamii nyingine kama Kiazeri (16%) na Kiarabu (2%) (angalia orodha ya lugha za Uajemi).

Dini

Uajemi iliwahi kuwa na dini zake za Uzoroasta na Umani.

Kuanzia karne ya 4 BK idadi ya Wakristo ilikua.

Tangu karne ya 7 Waarabu Waislamu walivamia Uajemi na kuifanya polepole kuwa nchi ya Kiislamu. Katika karne ya 16 Uislamu wa Kishia ulitangaziwa kuwa dini rasmi nchini.

Leo hii takriban asilimia 90 za wakazi ni Waislamu Washia. Karibu 10% ni Wasunni, hasa katika maeneo karibu na mipaka; kiutamaduni Wasunni wengi ni Wakurdi, Wabaluchi au Waturkomani.

Wafuasi wa dini nyingine kwa jumla ni kama 1% ya wakazi wote. Kundi kubwa ni Bahai lakini dini yao ilipigwa marufuku baada ya mapinduzi ya Kiislamu. Kundi linalofuata ni Wakristoː kati hao kundi kubwa ni Waarmenia, halafu Wakaldayo. Wayahudi wa Uajemi ni kundi kubwa kati ya nchi zote za Kiislamu wa mashariki ya kati (0.01%). Wazoroasta wamebaki pia (0.03%). Kundi dogo sana ni Wamandayo wanaoitwa pia wafuasi wa Yohane Mbatizaji.

Tazama pia

Tanbihi

Viungo vya nje

WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Nchi na maeneo ya Asia

Afghanistan | Armenia2 | Azerbaijan | Bahrain | Bangladesh | Bhutan | Brunei | China | Falme za Kiarabu | Georgia2 | Hong Kong3 | Indonesia | Iraq | Israel | Jamhuri ya China (Taiwan) | Japani | Kamboja | Kazakhstan | Kirgizia | Korea Kaskazini | Korea Kusini | Kupro2 | Kuwait | Laos | Lebanoni | Macau3 | Malaysia | Maldivi | Mongolia | Myanmar | Nepal | Omani | Pakistan | Palestina | Qatar | Saudia | Singapuri | Sri Lanka | Syria | Tajikistan | Timor ya Mashariki | Turkmenistan | Uajemi | Ufilipino | Uhindi | Urusi1 | Uthai | Uturuki1 | Uzbekistan | Vietnam | Yemen | Yordani

1. Nchi ina maeneo katika Asia na Ulaya. 2. Nchi iko Asia lakini inahesabiwa pia kati ya nchi za Ulaya kwa sababu za historia au utamaduni. 3. Eneo la pekee la China.